Friday, 9 October 2015

JIFUNZE KUSAMEHE NA KUSAHAU Mwalimu C.Mwakasege

            Tuna uhakika ya kwamba, Roho Mtakatifu anakuongoza kusoma somo hili kwa makusudi kamili.

            Maneno yaliyomo humu ni ya kukusaidia wewe na Wakristo wote, ili tuweze kuishi maisha ya "amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao."(Waebrania 12:14).
            Kusamehe na kusahau ni tatizo kubwa ambalo limewazuia wakristo wengi wasipokee majibu ya maombi yao toka kwa Mungu. Ninaamini kuwa maneno yaliyomo humu yatakusaidia katika kupokea majibu ya maombi mengi ambayo hujayapokea.
            Ni maombi yetu kwa Mungu, katika Jina la Yesu Kristo ya kwamba, Roho Mtakatifu ayachukue mafundisho haya na kuyaandika katika moyo wako, na akusaidie kuyatenda.
            Na unaposoma itakuwa ni vizuri ukiwa na Biblia yako karibu, ili usome mistari yote tuliyoiandika. Somo hili tutajifunza kwa wiki sita mfululizo. Somo la wiki inayofuata litakuwa linajenga juu ya somo la wiki linalotangulia hasa baada ya wiki ya kwanza.
 Mungu akusaidie unapofuatilia somo hili mpendwa wa mungu


KUTOKUSAMEHE NI KIKWAZO
" Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehi, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu" (Marko 11:25,26).

            Kutokusamehe ni kikwazo na kizuizi kikubwa ambacho kinasimama kati ya mtu na majibu ya maombi yake. Watu wengi wanapenda imani zao zikue, lakini kwa sababu ya kutokusamehe imani zao zinakuwa hazina matunda.
            Tatizo si kwamba watu hawapendi kusamehe. Ingawa watu wanapenda kusameheana, lililo wazi ni kuwa walio wengi hawajui namna ya kusamehe kule kunakokubalika na Bwana. Watu wengi wanajifunza katika biblia juu ya imani, maombi, utakatifu na mambo mengine ya kiroho. Lakini ni watu wachache wanaojifunza kutoka katika biblia namna ya kusamehe.Kati ya vizuizi vya mtu kupokea jibu la maombi yake kutoka kwa Mungu, ni tatizo la kutokujua jinsi ya kusamehe.
            Bwana Yesu alipowambia wanafunzi wake juu ya kusamehe alitaka waone uhusiano ulipo kati ya sala na kusamehe. Kwa maneno mengine alitaka wafahamu kuwa kujibiwa kwa maombi na sala na dua kunategemea sana uhusiano walionao na watu wengine.Kabla Yesu hajasema juu ya kusamehe alizungumza maneno muhimu sana juu ya maombi. Yesu alisema hivi:

" Mwamini Mungu. Amini, nawaambia, yeyote atakayeuambia mlima huu, ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu." (Marko11:22 - 24)

            Haya ni maagizo muhimu sana kwa kila mkristo, kwa ajili ya maisha ya ushindi kila siku. Na watu wengi wamekuwa wakiitumia mistari hii, ili kupata mahitaji yao ya kiroho na ya kimwili.
            Mafanikio yako katika kutumia mistari hiyo na ahadi hizo za Bwana Yesu, yatategemea sana jinsi wewe unavyofuata maagizo ya Yesu juu ya matumizi ya mistari hiyo.
            Kuna mtindo uliozuka katikati ya watu wa Mungu, wa kuifanya biblia kuwa kama duka. Wanafungua biblia, wanachagua mistari wanayotaka na ahadi wanazotaka, wanaondoka nazo, huku wakiiacha mistari mingine kwenye biblia.
            Lakini wanapoitumia hiyo mistari ya ahadi wanazotaka, na kuona hakuna matokeo yoyote, wanaona kama kwamba neno la Mungu limepungua nguvu.Hiyo si kweli. Neno la Mungu halijapungua nguvu zake wala halitakujapungua nguvu zake. Neno la Mungu hudumu milele.Kwa hiyo ni vizuri kusoma na kutafakari ahadi za Mungu juu ya maombi, lakini pia ni muhimu sana kuhakikisha kuwa unafuata maagizo yote ya utumiaji wa ahadi hizo.Kwa hiyo walio wengi. Maombi yao juu ya magonjwa, ndoa zao, wokovu wa ndugu zao na kadhalika, yamefungwa kwa kutotimiza maagizo haya ya Bwana Yesu.

"NINYI KILA MSIMAMAPO NA KUSALI, SAMEHENI, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu   aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehi, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu" (Marko 11;25, 26).

            Maombi yako hayajibiwi mara nyingi kwa sababu ya wewe kutosamehe wengine. Kwa maneno mengine Yesu alitaka tufahamu kuwa, tusipojifunza kusamehe wengine waliotukosea, tutabaki na dhambi mbele za Mungu.
Maana yake nini basi?
            Maana yake, kutokusamehe kunahesabiwa kuwa ni kosa mbele za Mungu, na ni dhambi inayotutenga na uso wa Mungu, ili tusijibiwe maombi yetu toka kwa Mungu.
        Kutokusamehe ni uasi Dhambi ni uasi (1 Yohana 3:4) Dhambi ni kuasi maagizo ya Mungu.

            Kama Mungu ameagiza kwa kinywa cha Kristo kuwa kabla hatujaomba lo lote, ni lazima tusamehe kwanza; inakuwaje basi, wewe unataka ujibiwe maombi yako kabla hujamsamehe mwenzako?
            Na kwa kutokusamehe umeasi agizo la Mungu, na kufuatana na waraka wa kwanza wa Yohana 3:4 umehesabiwa kuwa umetenda dhambi.Kwa hiyo unahitajiwa utubu juu ya kutokusamehe!
            Tuna uhakika kuwa wewe unayesoma hayo umewahi kuisema 'Sala ya Bwana' iliyoandikwa katika kitabu cha Mathayo, Sura ya 6:9-15.
            Hatujui kama unaelewa uzito wa maneno yaliyomo katika sala hiyo. Walio wengi wanaisema kwa sababu wameikariri, lakini si kwamba wameielewa maana yake.
            Katika sala hiyo, kuna maneno yanayohusu mambo ya kusamehe:
"Utusamehe deni zetu (makosa yetu) kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu (walio tukosea). (Mathayo6:12)

Tafakari hili neno 'kama'
            Utusamehe makosa yetu, kama sisi nasi tunavyowasamehe waliotukosea.Hii ina maana ya kwamba kipimo kile unachokipimia katika kuwasamehe wengine ndivyo na Mungu atakavyotumia kipimo hicho hicho kukusamehe wewe mambo uliyomkosea.Sasa elewa kwamba hakuna kusamehe kukubwa, wala kusamehe kudogo. Kutokusamehe ni kutokusamehe. Na kusamehe ni kusamehe. Mizani yake inapima kitu kizima, haipimi msamaha kidogo kidogo.

Yesu alilifafanua jambo hili aliposema:-
        "Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msiposamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu." (Mathayo 6:14,15).

Je, unaweza kusamehe bila kusahau?
        Tulipokuwa tunaongea na mama mmoja juu ya kumsamehe mume wake, ili ugonjwa wake upone, alituambia; "Mimi nilikwishamsamehe siku nyingi."
        Tukamuuliza; "Una uhakika?"
        Akasema, "Ndiyo, la sivyo ningekuwa nimekwishatengana naye"
        Tukamuuliza tena: "Kuna wakati wo wote huwa unawaza kuwa isingekuwa ni watoto mliozaa naye, ungeomba talaka au ungeondoka tu?
        Akasema; Ndiyo, tena mara nyingi."
        Tukamwambia: "Kusamehe kwako kuko wapi wakati bado unayahesabu makosa ya mume wako, kiasi ambacho ndoa imeshikiliwa na watoto badala ya kushikiliwa na makusudi ya Mungu?"
        Yule mama akashangaa.
        Kuna watu wengine wanasema wamesamehe wakati, bado kuna fundo na shina la uchungu katika mioyo yao. Kwa kinywa wanasema, wamesamehe, lakini moyoni bado hawajasamehe.
        Na kuwatambua watu wa namna hiyo ni rahisi sana.
Mtu huyo huyo akimkosea tena, utamsikia akilalamika akisema;
        "Mtu huyu nilimsamehe lile kosa la kwanza, tena amerudia. Kumbe mambo yalikuwa hayajaisha, ndiyo maana hata siku fulani alisema maneno fulani, ndiyo maana hata juzi alimgombeza mtoto wangu ......"
            Utaona mtu huyo akiyakumbuka yote mabaya ya nyuma ambayo mwenzake alimtendea. Wengine hata hudiriki kusema kuwa: "Nitamsamehe lakini sitasahau"
Sasa, hiyo siyo lugha ya watu wa Mungu, waliookolewa na kununuliwa kwa damu ya thamani ya Yesu Kristo.
            Hiyo ni lugha ya watu wasiomjua Mungu, watu wa ulimwengu huu. Na Biblia inatuambia kwamba sisi siyo wa ulimwengu huu. (Yohana 17:16).
Weka hilo katika roho yako. Wewe si wa ulimwengu huu, kwa hiyo lugha na maneno ya ulimwengu huu hayakuhusu. Zungumza lugha ya watu watakatifu wa ufalme wa Mungu ambao ndiyo wa uzao wako.
            Utawezaje kusema kuwa umemsamehe mwenzako wakati bado una uchungu naye moyoni mwako? Utasemaje umemsamehe wakati kila wakati unalikumbuka na kulisema kwa watu kosa alilokufanyia?
Utasema huko ni kusamehe ambako Mungu anataka ufanye, ili na yeye akusamehe.
La hasha!
            Kusamehe bila kusahau kosa ulilokosewa ni kusamehe kusikokamilika wala kukubaliwa mbele za Mungu. Kusema umesamehe huku bado una uchungu moyoni mwako, ni unafiki ulio wazi mbele ya Mungu.
Je! hujawahi kusoma mistari ifuatayo:
"Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu, na mtu akimfyolea ndugu yake itampasa baraza; na mtu akimwapiza itampasa jehanamu ya moto."(Mathayo 5:21, 22)
            Unaweza kuona jinsi Yesu Kristo alivyofananisha hasira hiyo iliyojaa moyoni mwako juu ya ndugu yako na uuaji. Na adhabu zake zinafanana.Sasa, utakuwa unajiuliza, inawezekana kwa vipi mtu kusahau mabaya aliyotendewa?Basi nakuhakikishia kuwa inawezekana kabisa! Kwa kuwa yote yanawezekana kwake aaminiye. Na imani huja kwa kusikia neno la Mungu (Warumi 10:17) Tatizo lako ni kwamba unaona kusamehe na kusahau ni vitu viwili tofauti, kwa hiyo unavitenganisha. Huwezi ukatenganisha kusamehe na kusahau. Kwa kuwa huwezi kusamehe bila kusahau; na huwezi kusahau bila kusamehe.
            Ufanyeje basi, uweze kusamehe na kusahau ili na Mungu naye akusamehe na kusahau makosa yako?
Ili tuweze kufahamu namna ya kusamehe na kusahau, ni muhimu tuielewe tabia ya Mungu juu ya jambo hili.
Usiache kusoma somo la Wiki ya Pili ili kuendelea na somo hili la Jifunze kusamehe na kusahau katika kipengele kinachosema



HASARA ZA KULIPIZA KISASI
            Usilipize Kisasi! Unasikia? Hata ikiwa umefanyiwa ubaya wa namna gani, Biblia inafundisha na inakusihi usilipize kisasi kwa huyo aliyekufanyia ubaya. Biblia inasema hivi:

"Wapenzi, msijilipizie kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu Mimi, Mimi nitalipa, anena Bwana" (Warumi 12:19)


            Kuna hasara zinazoweza kukupata ukiamua kulipa kisasi kwa mambo uliyofanyiwa ambayo hayakupendezi. Ikiwa ni masuala ya kikabila, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kidini, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kifamilia, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kikazi, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya uhusiano wako na majirani zako, usilipe kisasi.Ndiyo! Usilipe kisasi! Kwa nini? Kwa sababu "imeandikwa kisasi ni juu yangu Mimi; Mimi nitalipa, anena Bwana".
Lakini ikiwa utaona ya kuwa Mungu hawezi kukusaidia na ukaamua kujichukulia madaraka ya kujilipiza kisasi hasara zifuatazo hakika zitakupata!

Hasara ya Kwanza:
UTASHINDWA!

            Katika jambo lolote lile lililokukasirisha - liwe la kidini, au kikabila, au kifamilia, au kikazi, na kadhalika ukiamua kulipa kisasi utashindwa wewe kwa sababu vita hivyo si vya mwili na wala silaha ambazo Mungu amekupa si za mwili! Tunasema hivi kwa sababu katika 2 Wakorintho 10:3- 5 imeandikwa hivi:"Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi yamwili; maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome, tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo".

            Tena katika kitabu cha Waefeso 6:12 imeandikwa hivi: "Kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho".
            Uwanja wa mapambano uliyonayo ni "katika ulimwengu wa roho" na mapambano uliyo nayo "si juu ya damu na nyama" - ingawa unaona ya kuwa ni watu na ni binadamu kama wewe wanaokusonga - lakini fahamu hili ya kuwa wanatumiwa tu na ibilisi!
            Mbinu mojawapo ya shetani anayotumia akitaka kukuangamiza ni kukufanyia kitu kitakachokukasirisha ili uamue kujibu au kushindana kimwili kwa sababu anajua ukishindana "kimwili" au katika mwili utashindwa hakika, maana vita hivyo si vya mwili wala silaha ambazo Mungu amekupa si za mwili!

Hasara ya Pili:
MATATIZO HAYATAKWISHA!

            Kumbuka imeandikwa hivi katika kitabu cha Wagalatia 6:7; "Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote ampandacho mtu. Ndicho atakachovuna".
            Ikiwa umeamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule aliyekufanyia - ubaya hautakwisha, kwa sababu utavuna ulichopanda.Ndiyo maana imeandikwa hivi:"Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, mabaya
hayataondoka nyumbani mwake" (Mithali 17:13)

            Ukiamua kulipiza kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa nyumbani mwako - Biblia inasema "mabaya hayataondoka nyumbani mwako" Hii ndiyo maana matatizo mengi katika ndoa na katika jamii hayaishi - kwa sababu mtu akifanyiwa ubaya naye analipa kisasi.
            Ukiamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa nchini mwako ujue hakika mabaya hayataondoka nchini mwako. Hili ndilo lililowapata wenzetu wa nchi za Burundi na Rwanda - kulipizana kisasi - matokeo ni uhasama usiotaka kupotea - pamoja na juhudi zote za kimataifa kutafuta suluhisho.
            Ukiamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa kazini kwako - fahamu mabaya hayataondoka kazini kwako. Ikiwa ni shuleni - mabaya hayataondoka hapo shuleni.
            Tena hali ya mwisho inakuwa mbaya zaidi,kila wakati kisasi kinapoendelea kupandwa. Kwa sababu ukiwapa watu ubaya - nawe utapewa ubaya kwa; "kipimo cha kujaa na kushidiliwa, na kusukwa - sukwa - hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile upimacho ndicho mtakachopimiwa (Luka 6:38)
            Kumbuka ubaya haushindwi na ubaya mwingine, bali unashindwa na wema - kama vile dawa ya chuki si chuki bali upendo! Ndiyo maana Warumi 12:21 inasema; "Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema".

Hasara ya Tatu:
UNAMZUIA MUNGU KUKUPIGANIA

            Unaweza ukashangaa, lakini ndivyo ilivyo! Ukiamua kulipa kisasi juu ya tatizo ulilonalo - unamzuia Mungu asikusaidie kulitatua.Mungu hawezi kukusaidia kwa sababu imeandikwa "msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana, imeandikwa, kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana".
Neno "ipisheni" limeandikwa kwa sababu kulipa kisasi "kunazuia" ghadhabu ya Mungu isipigane upande wako! Tena si hivyo tu lakini ukilipa kisasi unaingilia kazi ambayo si yako! Ni kazi ya Mungu maana anasema "Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana" Ikiwa kisasi ni juu ya Mungu kulipa, basi huhitaji wewe kulipa. Je, tunakwenda pamoja katika hili?
            Hatua yako ya kulipa kisasi inazuia mkono wa Mungu kukupigania - kwa hiyo ipishe ghadhabu ya Mungu kwa kutokujilipizia kisasi!

Hasara na Nne:
UNAJICHUMIA DHAMBI!
            Unapoamua kulipa kisasi, unajichumia dhambi! Hii ni kwa sababu kulipa kisasi huja kwa njia ya chuki iliyojengeka ndani yako kwa ajili ya mambo mabaya uliyofanyiwa. Huwezi kulipa kisasi bila ya kumchukia huyo unayejilipizia kisasi kwake. Na Biblia inasema hivi:
"Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajuaya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake" (1 Yohana 3:15).
Umeona hilo! Chuki huzaa kisasi, na huzaa dhambi ya kuua! Na
Isaya 59:2b inasema; "dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia".
            Kwa hiyo kama umekwisha lipa kisasi au umekusudia moyoni mwako kulipa kisasi ni muhimu utubu ili Mungu akusamehe na mawasiliano yako na Yeye yawe mazuri.





HATUA TANO MUHIMU KATIKA KUSAMEHE
            Biblia inatuambia kwamba Mungu huyu ambaye amesema anafuta na kuyasahau makosa yetu, kwa ajili yake mwenyewe, anakaa ndani ya watu wote waliompokea. Hebu soma na kutafakari maneno yafuatayo:

            "Hapa mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno akafanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli. ...... Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake, waliozaliwa,si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu" (Yohana 1:1, 14, 12, 13).

            Yesu Kristo anapoingia ndani ya moyo wako, baada ya wewe kumwamini na kumpokea, unapewa uzima wa milele ndani yako, na unaanza maisha mapya.Imeandikwa kwamba, " Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya (2Wakorintho 5:17)
            Utu mpya unazaliwa ndani yako, maisha, mawazo, matendo, maneno, yanatakiwa kubadilika Yesu Kristo aingiapo ndani yako. Pia, kusamehe kwako kunabadilika kunakuwa kupya.Lakini utaona kwamba watu wengi waliozaliwa mara ya pili, na kumkiri Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wao, bado wanaendelea kusamehe kama zamani.
            Biblia inasema " ya kale yamepita, tazama!yamekuwa mapya"(2Wakorintho 5:17).
             Kwa maneno mengine ni kwamba kusamehe kwako ulivyokuwa unafanya zamani, hakuhitajiki tena, tazama! Kusamehe sasa ni kupya. Tabia ni mpya.Zamani ulisamehe lakini bado ulikumbuka makosa uliyofanyiwa. Tena ulisamehe si kwa ajili yako bali kwa ajili yake aliyekukosea na wakati mwingine ulitaka uthibitisho kwanza kuwa kosa hilo halitarudiwa na ndipo usamehe. Ni lugha ya kawaida kusikia mtu akisema 'nasamehe lakini sitasahau'.
            Katika maisha mapya utatakiwa usamehe na kusahau kwa ajili yako mwenyewe, ili kuomba kwako kusizuiliwe na baraka zako zisizuiliwe. Kwa kuwa imeandikwa hivi:
            "Yeye asemaye yakuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda" (1Yohana 2:6)
            Wewe unayesema kwamba una Kristo ndani yako, basi inakupasa kuenenda kama Kristo alivyoenenda alipokuwa hapa duniani katika mwili.Kwa kuwa Kristo alisamehe na kusahau, basi na wewe inakubidi kusamehe na kusahau.
            Hatua tano zifuatazo zitakupa msingi imara wa kuishi siku zote katika upendo na amani na jirani zako na ndugu zako. Na pia, zitafungua milango mipya ya uhusiano wako na Mungu utakaoinua huduma yako katika kumtumikia Mungu. Na zaidi ya yote zitakuweka huru na magonjwa mengi yanayokusumbua:

1. Fahamu kuwa si wewe bali Kristo.
            "Nimesulibiwa pamoja na Kristo, lakini ni hai, wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu" (Wagalatia 2:20)
            "basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu, yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu" (Wakolosai 3:1-3)

            Mistari hii michache ni baadhi tu ya ile inayotufunulia mambo yaliyofanyika ndani yetu tulipompokea Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wetu.Si wewe unayeishi, bali ni Kristo aliye ndani yako. Na uhai ulio nao sasa, baada ya kuzaliwa mara ya pili, unao katika imani ya Mwana wa Mungu.Soma tena mstari huu:-
            "..... Kwa maana mlikufa na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu."
           
"Kwa maana mlikufa." Utu wako wa kale, na mtu wa kale ndani yako alikufa siku ulipompokea Kristo maishani mwako. Kilichofuata ni uzima wa Kristo, katika utu mpya ukidhihirishwa katika maisha yako.Sasa unaweza kuelewa kwa nini Yesu Kristo alisema awachukiae ninyi, amenichukia mimi. ( Yohana 15 :18)
            Mtu akikufanyia ubaya, usione kuwa anakufanyia wewe, ona kama vile Mungu aonavyo kuwa, ubaya huo anafanyiwa Kristo aliye ndani yako.Mtu akikutukana, akikusemea mabaya, akikupiga, fahamu kuwa si wewe anayekufanyia hayo, bali Kristo aliye ndani yako!Kuthibitisha haya Biblia inasema:
"Vita hivyo si vyako ni vya Bwana" (2 Mambo ya Nyakati 20:15). Ukiwa na wazo hilo katika roho yako, chukua hatua ya pili ifuatayo:

2. Mpende adui yako Umuombee
            "Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako na umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi ...." (Mathayo 5:43, 44)

            Jambo ambalo liko wazi ni kwamba hakuna msamaha wa kweli pasipo upendo,
            "Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtuma Mwanae ..." (Yohana 3:16)
             Kilichomfanya Baba Mungu kumtuma Yesu Kristo duniani ni Upendo. Alitupenda sisi mno, alitupenda upeo wakati bado tulipokuwa tungali wenye dhambi. Na kuudhihirisha upendo huo, Yesu Kristo alizaliwa duniani na kufa masalabani ili sisi tupone.
             Msamaha wa kweli unadhihirisha upendo ulio ndani ya mtu. Pasipokuwa na upendo, kusameheana hakupo. Palipo na upendo wa kinafiki, pia pana kusameheana kinafiki.
            Kusameheana hakuonekani siku hizi, katika ndoa, kati ya ndugu, kati ya majirani, kati ya watu wa Mungu, KWA SABABU UPENDO WA WENGI UMEKWISHA POA!
            Watu siku hizi wanafanya kile ambacho Yesu Kristo aliwaambia wasifanye. Yesu alisema, " Wapendeni adui zenu." Lakini, unaona katika watu wa Mungu, chuki imejaa, ndoa zinaharibika kwa sababu ya chuki, undugu unakufa kwa sababu ya chuki. Na ni hao wanaosema kuwa wameokoka na Yesu Kristo yumo ndani yao. Usiwachukie wanaokuudhi, wapende.
            Yesu Kristo anakuambia watu wa dunia wanawapenda wanaowapenda na kuwachukia wanaowachukia, lakini wewe si wa dunia hii, wapende hata wale wanaokuchukia na ili kuonyesha kuwa unawapenda kweli, uwaombee!
            Kwa nini Yesu Kristo, alisema "Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi?"
Ni,
            "Ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je? Nao hawafanyi kama hayo?" (Mathayo 5:45- 47).
            Ulipompokea Kristo, ulipokea upendo mpya ndani yako, unaokuwezesha kufanya mambo ambayo mtu wa kale aliyekuwa ndani yako asingeweza kufanya. Mtu mpya ndani yako ana upendo mpya.

Upendo huu mpya, una tabia mpya, na mambo mapya.
            "Upendo huvumilia, hufadhili, upendo hauhusudu; upendo hautakabari; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli huvumilia yote; huamini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote"(1Wakorintho 13:4 - 8).

            Upendo huu umo ndani yako, na ndio unaokufanya uwe kiumbe kipya. Ni upendo ulio hai (Warumi 5:5)
            Ni upendo unamuondolea mtu chuki, uchoyo na ubinafsi.
Kwa upendo huu, Bwana Yesu anataka uwapende adui zako, na kuwaombea pia ili wasamehewe na Mungu juu ya makosa waliyoyafanya.
            Kwa upendo huu fanya yale ambayo ulikuwa huyafanyi zamani.
Kama ulikuwa husalimiani na adui yako, chukua hatua ya upendo, msalimie na ikibidi mtembelee nyumbani mwake. Kula pamoja naye, furahi pamoja naye, na omba pamoja naye.
            Kuna watu wengine hawasalimiani wala kutembeleana na wazazi wao, au baba au mama, kwa sababu ya mambo yaliyofanyika zamani ambayo hawakuyapenda.
            Sasa, chukua hatua waandikie barua, na uwatembelee kwa maana upendo wa Kristo umekuweka huru, na chuki na kinyongo.
Kumbuka unayafanya hayo kwa ajili yako mwenyewe ili maombi yako yakubaliwe mbele za Mungu.
            Nafahamu kwa jinsi ya mwili, na kwa kutumia akili ya kibinadamu hatua hizo ni ngumu kuchukua.
            Ni kweli, lakini kumbuka si wewe unayeishi, bali Kristo ndani yako. Na unayaweza yote (pamoja na kuwapenda adui zako) katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13)
            Upendo unavunja nguvu za uadui. Usimuone jirani au ndugu ni adui tena. Kama vile wewe ulivyo kiumbe kipya ndani ya Kristo, kwa jicho la upya huo waone adui zako kuwa ni rafiki. Anza uhusiano mpya nao.
            " Lakini nawaambia ninyi mnaosikia wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi" (Luka 6:27,28)

3. Samehe na Kusahau:
            Wakati fulani nilikuwa mahali nikifanya semina ya neno la Mungu. Mtu mmoja akanifuata na akaniambia anataka nimuombee.
Nikamuuliza; "Nikuombee nini?"
Akasema; "Mimi shida yangu ni kwamba naona imani yangu ni ndogo na haikui, na maombi yangu hayajibiwi. Kwa hiyo naona nina shida katika maisha yangu ya kiroho, uniombee".
             Inawezekana hata wewe una shida ya namna hiyo, kwa hiyo tafakari kwa makini maneno haya.
              Niliahidi kumuombea baadaye kwa maana muda ulikuwa umekwisha.
Siku moja nilipokuwa ninaomba kwa Mungu juu ya shida yake, Bwana akanijibu katika roho yangu kuwa:
            "Mtu huyo ana matatizo ya ndoa na kuna jambo lililomuudhi. Yeye anafikiri amesamehe, lakini bado ana uchungu moyoni mwake. Mwambie asamehe na kusahau na shida yake itakwisha".
            Nilipowasiliana naye juu ya jambo hili, alikubali kuwa, ni kweli mwenzie amekuwa akimkosea mara kwa mara katika ndoa yao. Lakini alisema amekwisha msamehe.
            Nikamuuliza; "Je! mbona basi kila mkikosana unakumbusha makosa ya nyuma?"
            Akajibu; "Ni kweli, sasa nifanyeje wakati naona kila wakati makosa aliyonifanyia nyuma yakinijia kichwani?"
            Hili ni tatizo la wengi. Na hujikuta wanasema wamesamehe kumbe bado. Msamaha si jambo la akili ni hatua ya rohoni. Ni uamuzi unaotoka ndani ya moyo wako.
            "Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, sikuambiii hata mara saba, bali hata saba mara sabini" (Mathayo 18:21, 22)

            "Na kama akikukosea mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba , akisema, nimetubu msamehe. Mitume wakamwambia Bwana tuongezee imani" (Luka 17:4,5).
            Mistari hii inatuonyesha jinsi kukua kwa imani, kunavyohusiana sana na kusamehe.
            Wanafunzi walimwambia Bwana Yesu, awaongezee imani. Kwa kuwa walifahamu kwamba, kwa uwezo wao wasingeweza kusamehe kama Kristo anavyotaka.
            Ni kweli kabisa.
            Kama vile unavyohitaji imani katika kuomba, vile vile katika kusamehe na kusahau unahitaji imani.
            Ulipompokea Kristo ulipokea kiasi cha imani (Warumi 12:3)
            Na ili iongezeke unahitaji kusoma neno la Mungu na kulitenda. Imani huja kwa kusikia Neno la Mungu. (Warumi 10:17).
            Imani ni ya rohoni na kusamehe ni kwa rohoni.
            Unawezaje kusamehe na usiyakumbuke uliyofanyiwa?
            Hilo ndilo tatizo kubwa alilokuwa nalo yule mtu aliyeniambia niomuombee. Na wengi pia wana tatizo la namna hii, na limekwamisha uponyaji na majibu mengine ya maombi yao, wameombewa mara nyingi, lakini bila mafanikio.
Kusamehe na kusahau ni kitendo cha imani ambacho ni budi kionekane kwa njia ya matendo ya mtu.
            Kusamehe ni uamuzi wa mara moja na kusahau ni vita vya imani.
Sasa, utaniuliza, Ndugu Mwakasege, utawezaje namna hiyo?
            Kabla sijakujibu, na mimi nakuuliza swali.
            Siku ulipotubu dhambi zako, ulikuwa na uhakika gani ya kuwa Mungu amekusamehe wala hazikumbuki dhambi zako tena?
            Utasema kwa kuwa ukitubu Mungu anasamehe.
            Ni sawa kabisa. Hata mimi nakubaliana na hilo.
            Lakini, je! Unaona kuwa Mungu anaweza kukuambia ufanye kitu ambacho anajua huwezi kukifanya?
            Hapana hata kidogo. Bwana wetu si dhalimu!
            Anafahamu kuwa WEWE MWENYEWE HUWEZI, LAKINI YEYE KWA KUWA YUMO NDANI YAKO ATAKUWEZESHA KUSAMEHE NA KUSAHAU.
            Unayaweza yote katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13)
Ukiisha amua kumsamehe mtu hakikisha kwamba hulisemi tena jambo hilo katika kinywa chako.
            Kumbuka kinywa kinanena yaujazayo moyo (Mathayo 12:34)
            Na hayo maneno ndiyo yamtiayo mtu unajisi (Mathayo 15:18 - 20)
            Usitafakari wakati wo wote ule, kosa ulilofanyiwa; mawazo mabaya yanapokujia juu ya kosa ulilofanyiwa, fahamu kuwa ni shetani na nafsi yako tu.
Biblia inasema mpingeni shetani naye atawakimbia (Yakobo 4:7)
Na wala msimpe nafasi (Waefeso 4:27)
            Mwambie shetani aondoke na mawazo yake, kwa kuwa hilo kosa umelisamehe na kulisahau.
        Na wakati huo utafakari nini?
            "Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote ya kupendeza, yo yote yenye sifa njema, ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, YATAFAKARINI YAYO" (Wafilipi 4:8)

            "Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili; bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha MAWAZO na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na TUKITEKA NYARA KILA FIKRA ipate kumtii Kristo" (2 Wakorintho 10:3 - 5)

            Kusahau ni vita vikali vya imani vinavyopiganwa katika mawazo yako. Unaposhinda vita hivi, unajikuta umepiga hatua kubwa ya imani!
KWA HIYO KUMBUKA:Unasamehe kwa ajili yako Mwenyewe.
Na unasahau makosa uliyokosewa kwa ajili yako mwenyewe.
            Kumbuka hili kila wakati, unamsamehe aliyekukosea na kuyasahau aliyokukosea kwa ajili yako mwenyewe.
            Na kila wakati wazo likija kukukumbusha kosa hilo likatae kwa Jina la Yesu. Na USIKUBALI KULISEMA TENA MAISHANI MWAKO.

4. Hasira ipeleke kwenye maombi
"Mwe na hasira, ila msitende dhambi jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi" (Waefeso 4:26, 27)

            Mwe na hasira, ila msitende dhambi, ni mstari ambao watu wengi wameutumia vibaya. Kutokana na maneno hayo wamefanya vitendo vingi viovu kwa mawazo, maneno na kwa matendo.
            Biblia haiwezi kujipinga yenyewe. Roho Mtakatifu ndiye aliyewaongoza watu kuandika maandiko hayo Matakatifu.
Lakini, soma mistari ifuatayo:
            "Uchungu wote na ghadhabu na HASIRA na kelele na matukano YAONDOKE KWENU" (Waefeso 4:31)
            "..... HASIRA ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu" (Yakobo 1:20)
            "Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya HASIRA watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu" (Wagalatia 5:19 -21)
            Hapa unaona jinsi hasira ilivyofananishwa na uchawi, uasherati, uadui, ibada ya sanamu, na mambo mengine kama hayo ambayo yanamzuia mtu asiurithi ufalme wa Mungu.
Na Yesu Kristo akikaza ubaya wa hasira alisema:
            "Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, kila amwoneaye ndugu yake HASIRA itampasa HUKUMU" (Mathayo 5:21, 22)

            Yesu anasema ukiwa na hasira unastahili hukumu, lakini Roho aliyesema ndani ya Kristo, ni huyo huyo aliyesema ndani ya Paulo kuwa, "Mwe na hasira, ila msitende dhambi".
            Je! Unafikiri biblia inagongana yenyewe? Hapana! Paulo alikuwa ana maana gani aliposema tuwe na hasira lakini tusitende dhambi? Unawezaje mtu ukawa na hasira lakini usitende dhambi?
            Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya magonjwa na hasira.
Ngoja nikueleze jinsi mimi yalivyonitokea.
Mara tu mimi nilipompokea Kristo katika roho yangu, kulikuwa na kitu kimoja kilichokuwa kikinisumbua. Ilikuwa mtu akiniudhi nilikuwa nakasirika haraka sana. Na wakati wote nitakuwa nalifikiria jambo hilo moyoni mwangu.
Mwisho wake nilikuwa naona uchungu unaingia moyoni mwangu.
Sasa kila mara nilipokasirika nilikuwa nashindwa kuomba na mara ninaanza kuumwa homa.
            Jambo hili lilinisumbua muda mrefu. Kila nikitubu na kumsamehe aliyenikosea, na kuliacha hilo mikononi mwa Mungu; ugonjwa niliokuwa nao ulikuwa unapona.
            Nilifahamu kitu kimoja kuwa nikiweza kulitatua tatizo la hasira, ugonjwa huo hautaniruida tena. Kwa kuwa ulikuwa unakuja mara tu nikikasirika.
Nikawa na tatizo la hasira mikononi mwangu.
            Kwa hiyo, nikamlilia Mungu katika maombi juu ya shida hii.
Watu wengi wanatatizo la namna hii, kila wanapokasirika juu ya jambo fulani, wanaugua. Utakuta wengi wakikasirika wanaumwa vichwa, vidonda vya tumbo, kifua, moyo, damu kwenda mbio, homa, na magonjwa mengine.
Tatizo si ugonjwa hapo.Tatizo ni hasira!
            Nilipokuwa nikiomba, Roho wa Bwana alinipa jibu na naamini kuwa kama nilivyosaidiwa mimi na wewe utapata msaada. Na ndiyo maana nimekushirikisha hili.
            Unapoona kuwa kuna jambo limekuudhi, usiwe mwepesi kujibu au kufanya kitu. Tulia kimya na tafuta nafasi uanze kuomba.
            Kwanza tubu kwa Baba juu ya kukasirika kwako, na pili, mwambie Baba jinsi unavyojisikia moyoni mwako, bila kumficha kitu, na tatu, mwombe kitu ambacho unataka akufanyie katika jambo hilo.
            Utajikuta unapoomba na kuumimina moyo wako kwa Bwana, Yeye ataichukua hiyo hasira uliyokuwa nayo na uchungu wote. Na badala yake anahuisha upya upendo mpya ndani ya moyo wako utakaokuwezesha kupita juu ya tatizo ulilo nalo.
            Ukiona bado hasira inatokea, ikemee kwa jina la Yesu, na itatoweka.
Paulo aliposema, Mwe na hasira, ila msitende dhambi hakuhalalisha ya kuwa hasira ni nzuri.
            Kwa maneno mengine alikuwa akisema kuwa unapopata uchungu kwa kuudhiwa angalia usifanye vitendo vitakavyomuaibisha Kristo.
            Kwa kuwa kuudhiwa kupo maadamu upo duniani, na kwa mtu wa Mungu maudhi yanazidi. Lakini Paulo anasema watu wajue namna ya kuishughulikia hasira inapokuja kutokana na maudhi.
Ndiyo maana aliendelea kusema:
"Jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka, wala msimpe ibilisi nafasi" (Waefeso 4:26,28)
            Usimpe ibilisi nafasi kwa kuiacha hasira ikazaa ugomvi, matusi na fitina.
Uchungu huo utautoaje?
            Usiupeleke kwa aliyekuudhi, wala usikae nao. Upeleke kwenye maombi na upendo utavuma baada ya Mungu kuondoa uchungu uliokuwa nao.
            Kuna wengine wanasema hasira aliyonayo ni ya ukoo kwa kuwa ndugu zake waliomtangulia wana hasira.
            Kuna wengine huwa wakikasirika kuna kitu kinapanda na kikifika shingoni kinamfunga asiseme, na anaanza kupumua kwa nguvu na wakati mwingine huanza kulia.
            Ukiona namna hiyo, chukua silaha mkononi ya Jina la Yesu na ukemee. Maana hiyo ni roho ya shetani iliyojifunika katika hasira.
            Hakuna hasira ya ukoo kwa watu wa Mungu, ambao ni uzao mpya katika uzao wa Mungu. Ukoo wako ni ukoo wa Mungu. Ni ukoo wa Upendo si wahasira.
            Baada ya mimi kuchukua hatua hizo, ule ugonjwa sijauona tena, na hasira sikuiona kunifuatafuata kwa kuwa niliacha kuwatizama watu kwa jinsi ya mwili, bali nilianza kuwatambua kwa jinsi ya rohoni (2Wakorintho 5:16)

5. Furahi siku zote.
            Siri ya ushindi katika matatizo yoyote, inatokana na furaha ya Kristo iliyo ndani ya mtu.
            Neno la Mungu linasema, "Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema, Furahini" (Wafilipi 4:4)

" Heri ninyi watakpowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia;kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu" (Mathayo 4:11, 12)

            Huu ni ujumbe mzuri sana wa Bwana Yesu, kwa mtu wake aliyesongwa na maudhi pamoja na makwazo mbali mbali.
            Inawezekana kuwa ndani ya nyumba yako una makwazo ya kila siku, kutokana na mume wako au mke wako ambaye hatembei katika nuru ya Kristo.
            Na pia, inawezekana unapata maudhi sana juu ya tabia za watoto wako, ambao hawaenendi katika kweli ya neno la Mungu. Inawezekana unapata maudhi shuleni au kazini.
            Hata kama umesongwa na makwazo na maudhi namna hiyo, Yesu Kristo , aliye bwana na Mwokozi wako, anakuambia. "FURAHI NA KUSHANGILIA".
Furahi na kushangilia katika Bwana siku zote na katika yote. Hii ndiyo siri ya ushindi.
Kwa nini ufurahi na kushangilia?:
            Kwa kuwa unafahamu kuwa mgomvi wako si mtu bali ni shetani. (Waefeso 2:1 - 3).
            Kwa kuwa unafahamu kuwa anayekuudhi si mume wako, wala mke wako, wala watoto wako, bali ni shetani anayewatumia kutaka kukukasirisha wewe, ili umkosee Mungu wako.
            Kwa kuwa unafahamu kuwa shetani ameshindwa; na wewe una mamlaka juu yake na maudhi yake yote (Luka 10:19)
Kwa hiyo ufanyeje?
Furahi na kushangilia moyoni mwako.
            Kumbuka kuwa Kristo aliye ndani yako ni mkuu kuliko shetani na makwazo yake na maudhi yake (1Yohana 4:4).
            Furahi na kushangilia unapoudhiwa, na mtolee Mungu shukrani kwa nyimbo za sifa.
            Fanya hivyo na hasira haitapata nafasi moyoni mwako, wala uchungu wo wote.
            Tumia tabia ya Kristo iliyo ndani yako ya kuwaombea wanaokuudhi, kama vile yeye alivyosema pale msalabani, "Baba uwasemehe kwa maana hawajui walitendalo".
Baada ya kufurahi na kushangilia na kusifu, kitu gani kinafuata?
"Upole wako ujulikane na watu wote" (Wafilipi 4:5)
Na upole ni tunda la Roho. Na kazi ya roho ya upole ni kutuliza maudhi. (Mhubiri 10:4)
            Wakati wa maudhi ndiyo wakati mzuri wa kumdhihirisha Kristo aliye ndani yako katika upole wote na utulivu.
            Usijisumbue na kuhangaika katika neno lo lote, bali katika kila jambo, kwa kusali na kuomba na kushukuru, haja yako na ijulikane na Mungu (Wafilipi 4:6).
Usiwe mwepesi kumwambia mtu maudhi ya nyumbani mwako, au ofisini mwako. Utajikuta umeingia katika kusengenya na hutafaulu kamwe kujifunza kusamehe.
Maudhi na makwazo yapeleke kwa Bwana. Yeye anatosha kukushindia.
            Fanya hivyo, na amani ipitayo akili na fahamu zote na maudhi na makwazo itakuhifadhi na kukufariji moyo wako siku zote katika Bwana (Wafilipi 4:7)
Nilikuwa mahali fulani nikifundisha neno la Mungu, na kila siku niliombea wagonjwa. Basi, siku moja mama mmoja alisimama kushuhudia alivyopona.
Na haya ndiyo aliyosema:
            "Nina uhakika kuwa ugonjwa huu niliokuwa nao ulikuja kwa sababu ya dhambi nilizokuwa nazo. Mimi sikushikwa na dhambi zingine kama wengine wanavyoshikwa. Mimi nilishikwa na dhambi hii.
            Mume wangu huwa hanipi fedha ya kununulia chumvi nyumbani. Basi nilichukia sana; na mimi nikipata fedha na kununua chumvi, naificha nje ya nyumba. Mimi na watoto tunakula chakula chenye chumvi. Mume wangu namtengea chakula kisichokuwa na chumvi.
            Na niliwambia watoto ye yote atakayesema hayo kwa baba yake atachapwa.Lakini nilipoanza kufanya hivyo nilianza kuugua mara kwa mara, na hapa kwenye mkutano huu nimekuja na mguu umevimba na kunisababisha nisitembee vizuri.
            Baada ya kusikia neno la Mungu nilifahamu kuwa ugonjwa huu nimeupata kwa sababu ya kosa hilo la kumkasirikia mume wangu.
            Nikamsamehe mume wangu. Nikatubu kwa Mungu. Na maombezi ya wagonjwa yalipofanywa nilijikuta nimeanguka chini. Nilipoamka nilikuta uvimbe mguuni umetoweka. Na sasa nimepona na natembea vizuri.
Nikirudi nyumbani nitamwambia mume wangu yote, na nitamwomba anisamehe".
            Hii ndiyo nguvu ya uponyaji ya neno la Mungu inayoshuka baada ya kusamehe. Roho zinapona, miili inapona na ndoa zinapona! Yule mama alisamehe kwanza ndipo akapokea uponyaji.
            Na wewe sasa, samehe na kusahau upokee uponyaji wako au upokee majibu ya maombi yako.
            Kumbuka kabla ya kusimama na kusali samehe kwanza. Hii ni kwa ajili yako mwenyewe, ili usamehewe na Mungu na upokee unaloomba siku zote

by C&D Mwakasege 



TABIA YA MUNGU YA KUSAMEHE NDANI YAKO
            Ulipompokea Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako, ulipokea tabia ya aina gani?
"  Bali wote waliompokea (Kristo) aliwapa uwezo wa  kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu." (Yohana 1:12,13)
            Ulipozaliwa mara ya pili kwa Neno la Kristo ulifanyika kuwa mtoto wa Mungu.
Watoto wa Mungu wana tabia ya namna gani?
            Kwa kuwa wamehamishwa toka ufalme mwingine na uzazi mwingine, na kuingizwa katika ufalme wa Mungu na uzazi wake (Wakolosai 1:13); watoto hawa wanatakiwa wawe na tabia nyingine.
             Kabla ya kuzaliwa mara ya pili, kabla ya kumkiri Kristo ya kuwa ni Bwana: ulikuwa na tabia ya dunia hii iliyoongozwa na mfalme wa dunia hii ambaye ni shetani.
             Ulipozaliwa mara ya pili na kuukiri wokovu katika Kristo, ulipokea tabia mpya inayoongozwa na Mungu mwenyewe aliye ndani yako.

"  Kwa kuwa uwezo wake wa Uungu umetukirimia  vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa (Utakatifu), kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno; za thamani,ili kwamba kwa hizo mpate kuwa Washirika wa TABIA YA UUNGU, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa." (2 Petro 1:3,4)
             Mistari hii inatuonyesha wazi kabisa kuwa kwa uweza ule ule uliokuwezesha kuwa mwana wa Mungu, unakuwezesha kuipokea tabia ya Mungu.
             Tabia ya Mungu iliyo wazi ni Upendo kwa kuwa Mungu ni Upendo
(1 Yohana 4:8)

             Ni upendo ambao huvumilia, hufadhili, hauhusudu, hautakabari, haujivuni, haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, hauoni uchungu, hauhesabu mabaya, haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli,huvumiliayote,huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote, haupungui neno wakati wowote.Kamailivyoandikwa katika (1 Wakorintho 13:4 - 8)
 Mungu anavyosamehe:
         Ndani ya upendo, kuna tabia ya kusamehe na kusahau. Ili kuifahamu zaidi na tuitafakari tabia ya Mungu ya kusamehe na kusahau. Mungu anasema hivi:

"  Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe; wala sitazikumbuka dhambi zako." (Isaya 43:25)
Na tuitafakari tabia hii ya Mungu katika mafungu mawili yafuatayo:
1. Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe; na;
2. Wala sitazikumbuka dhambi zako.


              Haya ni maneno ya Mungu ambayo aliyasema kwa kutumia kinywa cha nabii Isaya, kwa ajili ya watu, baada ya kufunga agano jipya katika damu ya Yesu Kristo pamoja nao. Kwa kuwa katika agano la kale makosa (au dhambi) yalikuwa hayafutwi ila yanafunikwa tu kwa damu ya wanyama waliotolewa sadaka (Waebrania 10:1 - 25)
             Lakini katika agano jipya, makosa yanafutwa kwa uwezo wa damu ya Yesu iliyomwagika msalabani.
             Kuna tofauti kubwa kati ya kuifunika dhambi kwa damu na kuifuta dhambi kwa damu. Unapofunika, kosa haliondoki linabaki pale pale, lakini linakuwa halionekani. Unapofuta, kosa linaondolewa kabisa, inakuwa kama hakuna kosa lililowahi kufanyika.
             Ukiwa darasani, mwalimu akifuta maandishi ya chaki ubaoni, ubao unabaki hauna maandishi; unakuwa safi. Lakini utakuta yale yaliyokuwa yameandikwa, ingawa hayapo ubaoni, katika akili za watu yanakuwa yapo. Na wakati mwingi inachukua muda kufutika mawazoni.
             Sasa, ile sehemu ya kwanza ya mstari, Mungu anasema anayafuta makosa yetu kwa ajili yake mwenyewe, Mungu hakusema "Anayafunika makosa," bali amesema, "anayafuta makosa".
Soma tena:
"Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe."
Soma na maneno haya:
"Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote" (1Yohana 1:9)
            Ukitubu dhambi zako kwa Mungu katika Roho na Kweli, Mungu anakusamehe, na anafuta dhambi zako na mbele yake unaonekana kama hukufanya kosa lo lote. Hivyo ndiyo maana ya kuhesabiwa haki mbele za Mungu katika Kristo. Kusamehe ni kufuta au kuondoa kosa na kulisahau au kutokulikumbuka tena.
 Kusamehe kosa = kufuta + kutokulikumbuka kosa
            Wakati huu tunatizama jinsi Mungu anavyotusamehe. Hatua ya kwanza anafuta kosa machoni pake.
             Kwa nini Mungu atusamehe?
             Kwa nini Mungu ayafute makosa yetu?
             Umewahi kujiuliza kwa nini Mungu aliamua kukusamehe mabaya yote uliyoyafanya maishani mwako?
             Watu wengine wanafikiri wokovu unakuja kwa kumpendeza Mungu kwa matendo yao. Na matokeo yake wanajihesabia haki wenyewe badala ya kuhesabiwa haki na Mungu.
             Utamsikia mtu anasema mimi sina dhambi, siibi, sizini, silewi, sijatengwa na kanisa, na naitunza Sabato kwa hiyo sina kosa kwa Mungu!
 Lakini neno la Mungu linatuambia mambo tofauti, kwa mfano neno linasema hivi:

" Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala SI KWA MATENDO, mtu awaye yote
 asije akajisifu (Waefeso 2:8,9)


            Kwa hiyo, unaona kuwa matendo yako peke yake hayawezi kukupa wokovu, na ondoleo la dhambi, bila ya imani ndani ya Kristo. Imani lazima iambatane na matendo. Imani pasipo matendo imekufa (Yakobo 2:26).
            Kitu kinachomfanya Mungu akusamehe si uzuri wa matendo yako; bali anakusamehe KWA AJILI YAKE MWENYEWE.
              Mungu anasema; "Mimi, naam, Mimi, ndimi niyafutaye makosa yako KWA AJILI YANGU MWENYEWE"
            Huu ndiyo upendo wa ajabu!
            Kumbuka si kwa matendo yako bali kwa ajili yake mwenyewe Mungu, unapata kusamehewa makosa yako.
Mungu akisamehe anasahau:
            Hatua ya pili ambayo Mungu anaichukua mara tu anapofuta makosa yako ni kuyasahau aliyokwisha yafuta.
            Yeye mwenyewe ameahidi kwamba ".... Wala sitakumbuka dhambi zako". WALA SITAKUMBUKA DHAMBI ZAKO!
            Ina maana kuwa Mungu akiisha kukusamehe kwa ajili yake mwenyewe; anafuta na kusahau makosa uliyofanya, anakuhesabia haki bure mbele zake. Unasimama ndani yake kama mtu ambaye hajawahi kufanya kosa wala dhambi yo yote.
            Sasa kama Mungu amekwishafuta na kuyasahau mambo uliyofanya kabla hujaokoka na ukatubu, kwa nini wewe unayakumbuka? Jifunze kujisamehe mwenyewe! Mungu akikusamehe na wewe jisamehe. Mungu asipoyakumbuka makosa yako, na wewe usiyakumbuke!
            Huduma za watumishi wengi zinakwama mara tu anapokumbuka mambo aliyoyafanya zamani au maneno aliyoyasema - hata kama wamekwishayatubia!
            Kwa sababu hiyo, badala ya kusonga mbele katika Bwana, anajikuta kila wakati wanatubu juu ya dhambi hiyo hiyo. Na wanakosa ujasiri wa kusimama mbele za Mungu, mbele ya shetani na mbele za watu.
            Kila wanapotaka kufanya kitu, shetani anawaletea wazo kuwa, bado hawajasamehewa kosa alilolifanya jana au juzi. Na kwamba haitakuwa rahisi kwako kupokea baraka toka kwa Mungu. Kwa hiyo watu hawo anaanza kutubu tena upya!


            Watu wengi hata sasa hawana uhakika kama Mungu amewasamehe juu ya makosa waliyoyafanya.
            Uhakika utaupata katika Neno la Mungu.
Mungu ameahidi kuwa ukitubu katika Roho na Kweli, unasamehewa.
(1Yohana 1:9)
            Paulo alifahamu siri hiyo ya kuyasahau mambo ya nyuma aliyomkosea Kristo, kwa kuwatesa wafuasi wa Yesu, kabla ya kuokoka kwake. Hii ilimsaidia kulitangaza Jina la Yesu bila yeye kujisikia vibaya moyoni mwake.
Kwa hiyo Paulo aliweza kusema:
"...... ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele, nakaza mwendo niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu" (Wafilipi 3:13,14)
            Ili uweze kusonga mbele katika wokovu, ni budi ujifunze kujisamehe na kuyasahau uliyoyafanya zamani.


Tabia hii unayo ndani yako:
            Kuyafuta makosa na kutoyakumbuka tena ni tabia ya Mungu ambayo imo ndani yako sasa.
            Ulipompokea Kristo moyoni mwako na kumkiri kuwa ni Bwana wa maisha yako, pia ulipokea ndani ya moyo wako tabia hii ya Mungu ya kufuta makosa na kutoyakumbuka.
            Hii ndiyo tabia inayotakiwa ionekane katika maisha yako unapokosewa na mtu.
            Tatizo la wengi ni kwamba wamekuwa viumbe vipya, lakini wanataka kutumia tabia yao ya zamani. Katika tabia ya zamani, walisamehe lakini hawakusahau walichokosewa. Tabia mpya ni kufuta makosa na kutoyakumbuka kabisa. Kwa hiyo na sisi tukikosewa tunatakiwa kusamehe na kusahau!
Hatua zifuatazo katika mfululuzo wa masomo yanayofuata wiki zijao zitakusaidia kuijenga na kuitumia tabia hiyo ya Mungu iliyo ndani yako. Tunaamini utakuwa pamoja nasi wiki ijayo ili kuendelea na somo hili - katika kipengele kinachosema
            Ulipompokea Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako, ulipokea tabia ya aina gani?
"  Bali wote waliompokea (Kristo) aliwapa uwezo wa  kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu." (Yohana 1:12,13)
            Ulipozaliwa mara ya pili kwa Neno la Kristo ulifanyika kuwa mtoto wa Mungu.
Watoto wa Mungu wana tabia ya namna gani?
            Kwa kuwa wamehamishwa toka ufalme mwingine na uzazi mwingine, na kuingizwa katika ufalme wa Mungu na uzazi wake (Wakolosai 1:13); watoto hawa wanatakiwa wawe na tabia nyingine.
             Kabla ya kuzaliwa mara ya pili, kabla ya kumkiri Kristo ya kuwa ni Bwana: ulikuwa na tabia ya dunia hii iliyoongozwa na mfalme wa dunia hii ambaye ni shetani.
             Ulipozaliwa mara ya pili na kuukiri wokovu katika Kristo, ulipokea tabia mpya inayoongozwa na Mungu mwenyewe aliye ndani yako.

"  Kwa kuwa uwezo wake wa Uungu umetukirimia  vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa (Utakatifu), kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno; za thamani,ili kwamba kwa hizo mpate kuwa Washirika wa TABIA YA UUNGU, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa." (2 Petro 1:3,4)
             Mistari hii inatuonyesha wazi kabisa kuwa kwa uweza ule ule uliokuwezesha kuwa mwana wa Mungu, unakuwezesha kuipokea tabia ya Mungu.
             Tabia ya Mungu iliyo wazi ni Upendo kwa kuwa Mungu ni Upendo
(1 Yohana 4:8)

             Ni upendo ambao huvumilia, hufadhili, hauhusudu, hautakabari, haujivuni, haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, hauoni uchungu, hauhesabu mabaya, haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli,huvumiliayote,huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote, haupungui neno wakati wowote.Kamailivyoandikwa katika (1 Wakorintho 13:4 - 8)
 Mungu anavyosamehe:
         Ndani ya upendo, kuna tabia ya kusamehe na kusahau. Ili kuifahamu zaidi na tuitafakari tabia ya Mungu ya kusamehe na kusahau. Mungu anasema hivi:

"  Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe; wala sitazikumbuka dhambi zako." (Isaya 43:25)
Na tuitafakari tabia hii ya Mungu katika mafungu mawili yafuatayo:
1. Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe; na;
2. Wala sitazikumbuka dhambi zako.


              Haya ni maneno ya Mungu ambayo aliyasema kwa kutumia kinywa cha nabii Isaya, kwa ajili ya watu, baada ya kufunga agano jipya katika damu ya Yesu Kristo pamoja nao. Kwa kuwa katika agano la kale makosa (au dhambi) yalikuwa hayafutwi ila yanafunikwa tu kwa damu ya wanyama waliotolewa sadaka (Waebrania 10:1 - 25)
             Lakini katika agano jipya, makosa yanafutwa kwa uwezo wa damu ya Yesu iliyomwagika msalabani.
             Kuna tofauti kubwa kati ya kuifunika dhambi kwa damu na kuifuta dhambi kwa damu. Unapofunika, kosa haliondoki linabaki pale pale, lakini linakuwa halionekani. Unapofuta, kosa linaondolewa kabisa, inakuwa kama hakuna kosa lililowahi kufanyika.
             Ukiwa darasani, mwalimu akifuta maandishi ya chaki ubaoni, ubao unabaki hauna maandishi; unakuwa safi. Lakini utakuta yale yaliyokuwa yameandikwa, ingawa hayapo ubaoni, katika akili za watu yanakuwa yapo. Na wakati mwingi inachukua muda kufutika mawazoni.
             Sasa, ile sehemu ya kwanza ya mstari, Mungu anasema anayafuta makosa yetu kwa ajili yake mwenyewe, Mungu hakusema "Anayafunika makosa," bali amesema, "anayafuta makosa".
Soma tena:
"Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe."
Soma na maneno haya:
"Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote" (1Yohana 1:9)
            Ukitubu dhambi zako kwa Mungu katika Roho na Kweli, Mungu anakusamehe, na anafuta dhambi zako na mbele yake unaonekana kama hukufanya kosa lo lote. Hivyo ndiyo maana ya kuhesabiwa haki mbele za Mungu katika Kristo. Kusamehe ni kufuta au kuondoa kosa na kulisahau au kutokulikumbuka tena.
 Kusamehe kosa = kufuta + kutokulikumbuka kosa
            Wakati huu tunatizama jinsi Mungu anavyotusamehe. Hatua ya kwanza anafuta kosa machoni pake.
             Kwa nini Mungu atusamehe?
             Kwa nini Mungu ayafute makosa yetu?
             Umewahi kujiuliza kwa nini Mungu aliamua kukusamehe mabaya yote uliyoyafanya maishani mwako?
             Watu wengine wanafikiri wokovu unakuja kwa kumpendeza Mungu kwa matendo yao. Na matokeo yake wanajihesabia haki wenyewe badala ya kuhesabiwa haki na Mungu.
             Utamsikia mtu anasema mimi sina dhambi, siibi, sizini, silewi, sijatengwa na kanisa, na naitunza Sabato kwa hiyo sina kosa kwa Mungu!
 Lakini neno la Mungu linatuambia mambo tofauti, kwa mfano neno linasema hivi:

" Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala SI KWA MATENDO, mtu awaye yote
 asije akajisifu (Waefeso 2:8,9)


            Kwa hiyo, unaona kuwa matendo yako peke yake hayawezi kukupa wokovu, na ondoleo la dhambi, bila ya imani ndani ya Kristo. Imani lazima iambatane na matendo. Imani pasipo matendo imekufa (Yakobo 2:26).
            Kitu kinachomfanya Mungu akusamehe si uzuri wa matendo yako; bali anakusamehe KWA AJILI YAKE MWENYEWE.
              Mungu anasema; "Mimi, naam, Mimi, ndimi niyafutaye makosa yako KWA AJILI YANGU MWENYEWE"
            Huu ndiyo upendo wa ajabu!
            Kumbuka si kwa matendo yako bali kwa ajili yake mwenyewe Mungu, unapata kusamehewa makosa yako.
Mungu akisamehe anasahau:
            Hatua ya pili ambayo Mungu anaichukua mara tu anapofuta makosa yako ni kuyasahau aliyokwisha yafuta.
            Yeye mwenyewe ameahidi kwamba ".... Wala sitakumbuka dhambi zako". WALA SITAKUMBUKA DHAMBI ZAKO!
            Ina maana kuwa Mungu akiisha kukusamehe kwa ajili yake mwenyewe; anafuta na kusahau makosa uliyofanya, anakuhesabia haki bure mbele zake. Unasimama ndani yake kama mtu ambaye hajawahi kufanya kosa wala dhambi yo yote.
            Sasa kama Mungu amekwishafuta na kuyasahau mambo uliyofanya kabla hujaokoka na ukatubu, kwa nini wewe unayakumbuka? Jifunze kujisamehe mwenyewe! Mungu akikusamehe na wewe jisamehe. Mungu asipoyakumbuka makosa yako, na wewe usiyakumbuke!
            Huduma za watumishi wengi zinakwama mara tu anapokumbuka mambo aliyoyafanya zamani au maneno aliyoyasema - hata kama wamekwishayatubia!
            Kwa sababu hiyo, badala ya kusonga mbele katika Bwana, anajikuta kila wakati wanatubu juu ya dhambi hiyo hiyo. Na wanakosa ujasiri wa kusimama mbele za Mungu, mbele ya shetani na mbele za watu.
            Kila wanapotaka kufanya kitu, shetani anawaletea wazo kuwa, bado hawajasamehewa kosa alilolifanya jana au juzi. Na kwamba haitakuwa rahisi kwako kupokea baraka toka kwa Mungu. Kwa hiyo watu hawo anaanza kutubu tena upya!


            Watu wengi hata sasa hawana uhakika kama Mungu amewasamehe juu ya makosa waliyoyafanya.
            Uhakika utaupata katika Neno la Mungu.
Mungu ameahidi kuwa ukitubu katika Roho na Kweli, unasamehewa.
(1Yohana 1:9)
            Paulo alifahamu siri hiyo ya kuyasahau mambo ya nyuma aliyomkosea Kristo, kwa kuwatesa wafuasi wa Yesu, kabla ya kuokoka kwake. Hii ilimsaidia kulitangaza Jina la Yesu bila yeye kujisikia vibaya moyoni mwake.
Kwa hiyo Paulo aliweza kusema:
"...... ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele, nakaza mwendo niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu" (Wafilipi 3:13,14)
            Ili uweze kusonga mbele katika wokovu, ni budi ujifunze kujisamehe na kuyasahau uliyoyafanya zamani.


Tabia hii unayo ndani yako:
            Kuyafuta makosa na kutoyakumbuka tena ni tabia ya Mungu ambayo imo ndani yako sasa.
            Ulipompokea Kristo moyoni mwako na kumkiri kuwa ni Bwana wa maisha yako, pia ulipokea ndani ya moyo wako tabia hii ya Mungu ya kufuta makosa na kutoyakumbuka.
            Hii ndiyo tabia inayotakiwa ionekane katika maisha yako unapokosewa na mtu.
            Tatizo la wengi ni kwamba wamekuwa viumbe vipya, lakini wanataka kutumia tabia yao ya zamani. Katika tabia ya zamani, walisamehe lakini hawakusahau walichokosewa. Tabia mpya ni kufuta makosa na kutoyakumbuka kabisa. Kwa hiyo na sisi tukikosewa tunatakiwa kusamehe na kusahau!
Hatua zifuatazo katika mfululuzo wa masomo yanayofuata wiki zijao zitakusaidia kuijenga na kuitumia tabia hiyo ya Mungu iliyo ndani yako. Tunaamini utakuwa pamoja nasi wiki ijayo ili kuendelea na somo hili - katika kipengele kinachosema


JE ALIYEKUKOSEA ASIPOKUOMBA MSAMAHA UFANYEJE?
"Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwana neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu" (Marko 11:25,26)
            Yesu Kristo aliyasema maneno haya kwa wanafunzi wake wa kwanza, alipokuwa akiwafundisha juu ya imani. Maneno haya ya Yesu Kristo, yanatuhusu hata sisi tulio wanafunzi wake siku hizi.Yesu Kristo katika maneno haya anazungumza na mwanafunzi wake aliyekosewa na mtu mwingine.Na katika somo hili, toka mwanzo tumechukua mtazamo huu wa Yesu Kristo; tunazungumza na mtu aliyekosewa na mtu mwingine.Somo hili lina maneno yenye mafundisho kwa mtu ambaye amekwazwa na mwenzake;mtu aliyefanyiwa kosa lolote lile.Kuna watu wengi sana wanaokosewa na watu wengine. Na tunaamini hata wewe kuna wakati fulani katika maisha yako umekwazwa na mtu mwingine.Katika ndoa makwazo yamekuwa kitu cha kawaida. Maofisini watu wanakosana kila siku. Hata na katikati ya watu wa Mungu, makwazo yanatokea mara kwa mara.Na sehemu mojawapo muhimu katika maisha ya mkristo ni maombi. Na ili tuwe na maisha ya maombi yenye mafanikio, ni lazima tuwe watu wenye tabia ya kusamehe waliotukosea.Yesu Kristo alijua jambo hili na umuhimu wa kusamehe KWANZA kabla ya kuanza kuomba.Yesu Kristo alisema, " Ninyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu".Maneno haya hayatupi uchaguzi wa kusamehe mtu wakati tunapopenda tu au wakati tunapotaka.Maneno haya ni agizo la Bwana Yesu Kristo ambalo linatakiwa lifuatwe na kila mwanafunzi wake, ili aweze kuwa na mafanikio katika maombi yake.

Unatakiwa kusamehe mara ngapi?

            Mama mmoja ambaye alikuwa ana matatizo katika unyumba wake, alisikika akisema maneno haya:"Mume wangu amenitesa kwa muda mrefu sasa; na hali ya mambo ilivyo, sidhani kama naweza hata kumsamehe tena; maana nimemsamehe nimechoka".Ni kweli kabisa kwamba mtu mwingine anaweza kukukosea mara nyingi sana. Hii huwa mara nyingi inatokea kwa watu ambao wanakaa pamoja au ni majirani.Hali ya mama huyu aliyesema maneno hayo, inawapata watu wengi sana, na nina uhakika watu hao wamechoka na hali hiyo.
            Inawezekana wewe ni mke wa mume ambaye ni mlevi, malaya, na mgomvi. Kila akirudi nyumbani ni kukutukana na hata wakati mwingine kukupiga. Na umeomba kwa Mungu juu ya jambo hili kwa muda mrefu bila kuona mafanikio.Sasa umeamua ufanyaje wakati unaona unazidi kuonewa na kuteswa? Inawezekana wewe ni mume wa mke ambaye ni mlevi, malaya na mgomvi. Inawezekana wewe ni mzazi wa watoto ambao hawakusikii, walevi, malaya, na wahuni.Inawezekana wewe ni mfanyakazi katika ofisi ambayo unaonewa haki zako za kupanda cheo, kupanda mshahara na marupurupu mengine, bila sababu yoyote.Sasa, nakuuliza, umeamua kuwachukulia hatua gani hao watu waliokukosea?Kumbuka wewe ni mkristo, na unatakiwa uamue mambo yako kikristo, kwa kulifuata Neno la Mungu.Hawa watu wanaotukosea tunatakiwa kuwasamehe mara ngapi? Hili swali ni muhimu, kwa kuwa watu wengine hawachoki kuwakwaza wengine!
Imeandikwa:"Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye;akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba,akisema, Nimetubu, msamehe" (Luka 17:3,4):
            Ni kweli kabisa! Mtu akikukosea na akitubu ni rahisi kumsamehe. Lakini ikiwa mtu aliyekukosea asipokuja kutubu je naye anahitaji kusamehewa?Hata asipotubu msamehe.Hili ni jambo ambalo inabidi tulizungumze kwa kufuata Neno la Mungu; maana ni jambo linalowasumbua wengi.Kuna wakati fulani tulikuwa tunalijadili jambo la kusamehe na wenzetu. Mmoja kati ya wale waliokuwepo alisema hivi: "Mimi siwezi kumsamehe mtu aliyenikosea asipokuja kutubu".Inawezekana hata wewe una mawazo kama haya. Lakini nakuuliza swali hili, "Je, kuna mstari wo wote katika biblia unaosema mtu aliyekukosea asipotubu usimsamehe?".

            Sisi hatujawahi kuuona. Kama upo tunaomba utuambie.Huhitaji kuombwa msamaha ili upate kusamehe. Biblia inasema; ‘Utusamehe deni zetu, kama sisi tuwasamehevyo wadeni wetu’ Biblia haikusema ‘Utusamehe deni zetu, kama sisi tuwasamehevyo waliotuomba msamaha!Kwa hiyo tunatakiwa kuwasamehe waliotukosea hata kama hawakutuomba masamaha.Hii ni kweli. Na sasa tuone neno la Mungu linatuambia nini:
"Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana,ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, si kuambii hata mara saba,bali hata saba mara sabini" (Mathayo 18:21,22)
            Hapa hatuoni Yesu Kristo akimwambia Petro kuwa mtu ni lazima atubu ili asamehewe. Ila anamjibu kuwa "Sikuambii hata mara saba, bali saba mara sabini"Petro alifahamu ya kuwa anahitaji kusamehe hata asipoombwa msamaha. Tatizo lake lilikuwa ni asamehe mara ngapi.Kumbuka ya kuwa unayaweza mambo yote, pamoja na kusamehe bila kuombwa msamaha, katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13) Tena kumbuka ya kuwa ni tabia ya Mungu iliyo ndani yako (2Petro 1:3,4) inayokuwezesha kusamehe na kusahau hata kama hujaombwa msamaha.Kumbuka si wewe unayekosewa na kukwazwa, bali Kristo aliye ndani yako. Kwa kuwa ulipompokea Kristo katika moyo wako, ulifanyika kuwa kiumbe kipya. Si wewe unayeishi, bali Kristo ndani yako (Wagalatia 2:20)
MUNGU ALITUSAMEHE KABLA SISI HATUJAMUOMBA MSAMAHA WALA KUTAMBUA KOSA LETU.MUNGU ALITULIPIA DENI LETU LA DHAMBI KABLA SISI HATUJAMUOMBA MSAMAHA.
Kwa maana imeandikwa: "Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi" (Warumi 5:8)."…….Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa tungali wenye dhambi". Maana yake tulipokuwa bado hatujaomba msamaha Yesu alikufa kwa ajili yetu. Mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23). Na kwa kufa Kristo inamaanisha tumesamehewa na kulipiwa deni letu. Kazi tunayotakiwa kuifanya ni kuupokea msamaha kwa njia ya toba.
            Hata Yesu Kristo alipoteswa na kusulubiwa, na kufa msalabani, aliwasamehe waliomsulubisha na akawaombea msamaha (Luka 23:34); KABLA ya kuombwa msamaha.Na ni sauti ya Yesu Kristo inayosema ndani yako ukikosewa na mtu; "Msamehe kwa kuwa hajui alitendalo". Na Yesu akisema msamehe mtu, basi huna budi kusamehe.Na kumbuka unatakiwa kusamehe KWA AJILI YAKO MWENYEWE, hata kama hujaombwa msamaha ili na wewe usamehewe na Mungu. Usiposamehe unazuia maombi yako yasijibiwe na unazuia baraka zako zingine.

SOMO LA PILI


NANI ANAUPENDA WOKOVU WA KIMASIKINI?
            “Nani anaupenda wokovu wa Ukristo wa kimaskini?” Ukiona mtu amefika hali ya kujiuliza swali la jinsi hii, ujue ana hali ngumu sana kiuchumi.

            Hili swali nilijikuta najiuliza mwenyewe baada ya kuwa na hali ngumu sana kimaisha baada kuokoka. Kuna wakati fulani baada ya kuokoka mimi na mke wangu tulijikuta tumefika mahali pa kukosa hata dawa ya mswaki, nguo, viatu, na chakula kizuri. Licha ya shida hizi zote bado zilifuata zingine baada ya ndugu zetu wawili tuliokuwa tunawalipia masomo yao kufukuzwa na kurudi nyumbani kwa kukosa ada. Na waliambiwa wasirudi shuleni bila nusu ya ada!

            Unadhani tulikuwa na furaha tena? Ingawa tulikuwa tunasema tumeokoka, na mtu akituambia ‘Bwana asifiwe’ tuliitika ‘Amina’ ndani ya mioyo yetu tulikuwa na vita vikali na maswali mengi.

            Ni vigumu kuieleza hali hiyo tuliyoipitia ilivyokuwa ngumu kwa maneno. Lakini utaelewa mtu mwenye familia anavyojisikia anapoona anakosa hata fedha za kuwanunulia mke na watoto wake chakula licha ya mavazi. Wakati huo tulikuwa na mtoto mmoja.

            Hali ilivyozidi kuwa ngumu, ndivyo nilivyozidi kusongwa na mawazo. Ilifika wakati ambapo nilikuwa naona aibu hata kukaa sebuleni, maana niliogopa hata kuwaangalia wale vijana waliofukuzwa shule, nikijua kuwa wataniangalia kwa macho ya huruma ili niwape ada warudi shule. Lakini si kwamba nilikuwa siwahurumii, bali sikuwa na fedha za kuwapa.

            Ningeanzaje kuwaambia kuwa sina fedha, wakati wanajua nafanya kazi, na pia waliona nilikuwa na fedha nyingi kabla sijaokoka? Jambo hili lilinifanya niwaze sana. Inakuwaje kabla sijaokoka nilikuwa na fedha nyingi na baada ya kuokoka najikuta nimefilisika? Ingawa ni kweli kwamba kabla ya kuokoka fedha zingine nilizipata kwa njia zilizo kinyume cha ukristo lakini nilikuwa nazo. Na baada ya kuokoka ilibidi niziache njia hizo – na matokeo yake nilijikuta nimefilisika.

            Lakini nilikuwa nimesoma katika Hagai 2:8 kuwa fedha na dhahabu ni mali ya Mungu. Na pia nilijua kuwa vyote vya Mungu ni vyangu nikiwa ndani ya Kristo. Kwa hiyo ilikuwa vigumu kuelewa kwa nini Mungu aseme fedha ni mali yake, halafu mimi niliye mtoto wake nisiwe nazo.

            Ningewezaje kusema wokovu ni mzuri wakati baada ya kuokoka nimejikuta sina fedha za kutosha kununua chakula, nguo, dawa ya mswaki na hata kukosa ada za watoto! Je ndivyo Mungu anavyotaka tuwe baada ya kuokoka?

            Wakati huo ndipo nilipoelewa kwa nini wana wa Israeli waliyakumbuka masufuria ya nyama ya Misri, ingawa walikula nyama hizo wakiwa utumwani. Ni rahisi sana mtu aliyeokoka kurudia njia au maisha mabaya ya kutafuta fedha kwa njia zilizo kinyume cha ukristo anapokuta anabanwa na matatizo ya kiuchumi maishani mwake. Na hata wakati mwingine unakesha katika maombi ili kumlilia Mungu akupe chakula na mavazi unaona kama vile hasikii.

            Nilipokuwa nasumbuliwa na hali hii ndipo nilipojikuta najiuliza mwenyewe; “ Nani anaupenda wokovu wa kimaskini?” Nilijikuta siupendi kabisa. Ni wokovu gani huu ambao haunisaidii hata kutunza familia yangu?

            Siku moja nilimuuliza mke wangu; nikasema; “Je! wewe unaupenda wokovu wa kimaskini?”

            Akajibu; “Hapa, siupendi!”

            Nikasema; “Naona tuna mawazo yanayofanana. Kwa hiyo naona ni muhimu tumuulize Mungu katika maombi kwa nini tulipokuwa kwa shetani tulikuwa na fedha za kutosha, lakini baada ya kuokoka na kuja kwake tunajikuta hatuna fedha hata za kununulia vitu muhimu?”

            Baada ya kukubaliana hayo, mimi na mke wangu tulianza kumwomba Mungu kwa mfululizo wa siku tatu juu ya jambo moja hilo hilo. Namshukuru Mungu kwa kunipa mke ambaye aliweza kusimama pamoja nami katika maombi juu ya jambo hili. Sijui ningekuwa na hali gani kama angelalamika. Namshukuru Mungu mke wangu hakulalamika bali ALIOMBA PAMOJA NAMI.

            Mungu alitujibu maombi na akaanza kutufundisha mambo mengi ambayo mengine nawashirikisha katika ujumbe huu.

            Tulijua hakika kuwa hayakuwa MAPENZI YA MUNGU tuwe na hali ngumu ya kimaisha namna hiyo – kukosa fedha za kutosha kununulia nguo, chakula na vitu vingine muhimu. Na baada ya kuyaweka katika matendo yale tuliyoambiwa na Bwana yaliyo katika neno lake, hali yetu ilibadilika. Na matatizo tuliyokuwa nayo wakati ule yakaisha. Tukaanza kuona furaha tena katika maisha haya ya wokovu.

            Ni vizuri kujua kuwa Mungu wetu hapendi tuwe maskini. Wala hapendi wokovu wa kimaskini! Ndiyo maana alimtuma Mwana wake wa Pekee, Yesu Kristo kutukomboa.

            Kwa kukumbusha tu, Yesu Kristo aliyafanya yafuatayo kwa kufa na kufufuka kwake:

            "Yesu Kristo alifanyika dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tuhesabiwe haki bure ndani yake ya kusimama tena mbele ya Mungu"
(2Wakorintho 5:21)

            "Yesu Kristo aliuchukua udhaifu wetu, ili katika mambo yote tuzitegemee nguvu zake" (Mathayo 8:17; Wafilipi 4:13)
            Yesu Kristo aliyachukua magonjwa yetu, ili tusitawaliwe na magonjwa tena na kwa kupigwa kwake tumepona (Isaya 53:4,5; Mathayo 8:17; 1 Petro 2:24)
Yesu Kristo aliyachukua masikitiko na huzuni zetu, ili tukae katika amani yake ipitayo fahamu zote (Isaya 53:34; Wafilipi 4:6,7)
            Yesu Kristo alikuwa maskini kwa ajili yetu ingawa alikuwa tajiri, ili sisi tupate kuwa matajiri katika Yeye (2 Wakorintho 8:9)

Ndiyo maana matunga Zaburi 23 aliandika hivi:

“Bwana ndiye mchungaji wangu, SITAPUNGUKIWA NA KITU.Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake …. Hakika WEMA
NA FADHILI zitanifuata siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele”.

            Ni rahisi sana kusema. “Bwana ndiye mchungaji wangu, SITAPUNGUKIWA NA KITU, lakini je! Ni kweli hujapungukiwa na kitu? Je! Zaburi hii ni ya kweli, au ni maneno mazuri tu ya kutungia nyimbo?

            Lakini napenda kukutia moyo kuwa maneno haya ni ya kweli, ukikaa ndani ya Kristo hutapungukiwa na kitu. Ndiyo maana Mungu alimwambia Yoshua ya kuwa atii maagizo yake yote na kuyafanya HATAMPUNGUKIA WALA KUMUACHA (Yoshua 1:5)

            Kwa kuwa maneno haya ni ya kweli, mbona basi wakristo wengi WAMEPUNGUKIWA NA VITU? Tatizo haliko kwa Mungu, bali kwetu sisi. Na tuwe watendaji wa neno na tutaona mafanikio.


WAJIBU WA WAKRISTO:
            Ni wajibu wa wakristo (a) kusaidiana sisi wenyewe kiuchumi; na (b) Kuwasaidia kiuchumi watu wengine wasio wakristo. Kuna wakati fulani mtu mmoja alikuja kwangu kuomba ushauri.

            Nikamuuliza. “Una tatizo gani linalokukabili?”

            Akasema; “ Baada ya kuokoka ilibidi niache njia fulani fulani ambazo zilikuwa zinanisaidia kupata fedha kwa kuwa zilikuwa ni kinyume cha maadili ya kikristo. Lakini sasa naona napata shida, sina fedha za chakula, wala sijui kodi ya nyumba mwezi huu nitapata wapi. Licha ya hayo, wale niliowakopa fedha kufanyia biashara hizo nilizoziacha wananidai fedha zao. Hata naogopa kukutana nao. Hebu nisaidie mawazo, najua nimeokoka kweli, lakini NITAISHIJE KATIKA HALI HII?”

            Unadhani swali lilikuwa jepesi kujibu? Si swala la kumwambia tuombe halafu umwache aende zake! Yeye anachotaka baada ya kuomba aone msaada unamjia. La sivyo maombi hayo yanakosa maana kwake.

            Swali hili “Nitaishije katika hali hii?” Linawasumbua walio wakristo wengi siku hizi. Na umefika wakati wa kulijibu.

            Ngoja nikuulize swali jingine. Unadhani mwanamke ambaye anafanya uasherati ili kupata fedha za kuwalishia watoto wake hajui kuwa uasherati ni dhambi? Nina uhakika anajua kwa kuwa kuna mwingine hata kama anafanya hayo hakosi kila jumapili kanisani, na wakati mwingine hutoa sadaka kwa fedha hiyo hiyo. Unadhani hajui kuwa uasherati ni dhambi? Unadhani hamwelewi mchungaji anaposema acheni dhambi? Unadhani haogopi magonjwa ya zinaa? Unadhani anapenda kufanya hivyo? Nina hakika walio wengi hawapendi kufanya hivyo. Lakini jambo linalomsumbua, akiacha uasherati atapata wapi fedha za kuwatunza watoto wake? Nina uhakika akijibiwa swali hili ni rahisi kuacha tabia hiyo chafu.

            Wasichana wengi mashuleni wamejikuta wamebeba mimba na kuharibu usichana wao kwa kudanganywa na fedha wanazozihitaji kwa ajili ya kununulia mafuta ya kupaka, nguo, na kutengeneza mitindo ya nywele.

            Vijana wengi wa kiume wamejikuta wamejiingiza katika biashara haramu kwa sababu ya kutaka utajiri wa haraka haraka.

            Kwa sababu ya kutokujua la kufanya wakristo wengi wamepoteza ushuhuda wao kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi.

            Wakristo wenzetu walifanyaje? Tusome kitabu cha Matendo ya Mitume 4:32,34,35.

            “Na jamii ya watu waliamini (Wakristo) walikuwa na MOYO MMOJA NA ROHO MOJA; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na VITU VYOTE SHIRIKA. WALA HAPAKUWA NA MTU MMOJA MIONGONI MWAO MWENYE MAHITAJI; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa; wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa KWA KADRI YA ALIVYOHITAJI”

            Utaona katika habari hii ya kuwa kwa sababu ya Ukarimu na kutokuwa na ubinafsi wakristo hao waliweza kupambana na tatizo la umaskini katikati yao. Ndiyo maana ikandikwa kuwa; “WALA HAPAKUWA NA MTU MMOJA MIONGONI MWAO MWENYE MAHITAJI”. Jina la Bwana libarikiwe!

            Matokeo ya usharika namna hii ni haya; “Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote” (Matendo ya Mitume 4:33)

            Je! Siku hizi hakuna wakristo wenye mahitaji kati yetu? Na tunafanya nini ili kuwasaidia? Je! Kuwaombea tu kunatosha? Je! Unashangaa kwa nini ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu hautangazwi kwa nguvu na wakristo? Nadhani wakristo wengi wanatumia muda wao mwingi sana kujitafutia mahitaji yao kiasi ambacho muda unaobaki hautoshi kufanya kazi ya kushuhudia.

            Wenzetu walisaidiana, na sisi tusaidiane. Wazazi mara nyingi huwa wanawasaidia vijana wao waliowaoza kuanza maisha mapya. Na fahamu kuwa wokovu ni maisha mapya. Tunawajibika sana kuwasaidia wale wanaookoka kiroho na kimwili kuanza maisha mapya ndani ya Kristo. Kwa kukosa msaada wa kiuchumi, wengi wamepoa na kurudi nyuma.

            Niliwahi kushirikishwa ushuhuda mmoja ambao naamini utakusaidia kukuelewesha jambo hili ninalokuambia.

            Kuna mtu mmoja aliokoka baada ya muda mrefu kuwa mganga wa kienyeji na mchawi. Baada ya kuokoka ilibidi aache uchawi na uganga wa kienyeji, shughuli hizi ndizo zilizokuwa zinamsaidia kupata fedha ya matumizi.

            Baada ya kukaa miezi michache katika wokovu, bila ya kuwa na njia nyingine ya kupata fedha, ilibidi atumie akiba yote aliyokuwa nayo. Baada ya hiyo akiba kuisha akaanza kupata shida namna ya kuishi.

            Akiwa katika mahangaiko hayo, wakaja watu nyumbani kwake wakiomba msaada wa kutibiwa magonjwa yao. Hao watu walisikia kuwa yeye ni mganga wa kienyeji, wala hawakujua kuwa alikuwa ameokoka na kuacha uganga huo.

            Kwa sababu ya kukosa fedha, huyo mtu aliyeokoka akawaza moyoni mwake; “Hawa watu hawajui kuwa nimeokoka, kwa hiyo hakuna haja ya kuwaambia, kwani kuna ubaya gani nikienda kuwachimbia dawa ninazozifahamu halafu wanipe fedha inisaidie?”

            Kwa hiyo akaenda akawachimbia hizo dawa akawapa. Na hao watu wakaondoka baada ya kumlipa fedha. Lakini usiku, huyo aliyeokoka alipokuwa amelala aliona katika maono. Katika maono hayo akayaona majini mawili yaliyokuwa yanamsaidia katika uchawi zamani kabla ya hajaokoka. Hayo majini yakasema; “Tulikwaambia hutafanikiwa katika wokovu, sisi ndiyo tumekufilisi mali yako. Na pia sisi ndiyo tuliowatuma wale wagonjwa waje kwako. Ulipochima zile dawa ukatuita tulikokuwa. Sasa tumekuja, mwache Yesu njoo kwetu nasi tutakutajirisha”.

            Huyo mtu aliyeokoka aliposikia hayo, akatambua kosa lake, na mara hiyo akalikumbuka jina la Yesu Kristo. Kwa hiyo akayakemea yale majini nayo yakatoweka. Akamka akiwa anatetemeka.

            Kama asingelikumbuka uwezo wa jina la Yesu Kristo, angefanya nini? Naamini kama angepata msaada wa mahitaji yake toka kwa wakristo wenzake, asingebanwa na mtego huo. Wakristo naomba kuwakumbusha kusaidiana. Ni muhimu sana kwa maisha yetu ya kila siku.

            Ndiyo maana Mtume Paulo aliongozwa na Roho Mtakatifu kuandika hivi:

            “Kwa habari za kuwahudumia watakatifu (Wakristo) sina haja ya kuwaandikia. Maana najua utayari wenu, ninaojisifia kwa ajili yenu kwa Wamakedonia, kwamba Akaya ilikuwa tayari tangu mwaka mzima; na bidii yenu imewatia moyo wengi wao ……. Maana utumishi wa huduma hii hauwatimizii watakatifu (Wakristo) riziki walizopungukiwa tu, bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu, kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo, wanamtukuza Mungu kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote” (2Wakorintho 9:1,2,12 – 15)

            Ndiyo maana pia katika makanisa kuna mgawanyiko wa huduma. Kuna wengine kazi yao ni kuhubiri na kuwaambia watu waache dhambi kama, uasherati na wizi. Ni wajibu wa wale wanaoshughulika na mambo ya miradi ya maendeleo katika kanisa ni kusaidiana na wahubiri hao kuwaongoza watu waishije baada ya kuacha uasherati na wizi.

            Napenda kukuhimiza hata wewe unayeyasoma haya kuwa, ukiona mwenzako ni mhitaji wa kitu fulani ambacho unacho, usisite kumsaidia. Kumbuka huduma hii ina thawabu yake kama Mtume Paulo anavyosema.

            Hebu jibu swali hili; “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?" (1Yohana 3:17)

            Mzee Yohana anatushauri anasema, “Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli” (1Yohana 3:18).

            Ni kweli Bwana Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alikuwa maskini, lakini baada ya kufufuka alirudishiwa utajiri wake. Ndiyo maana Mtume Paulo anazungumzia juu ya “……… utajiri wake Kristo usiopimika” (Waefeso 3:8). Na katika Wafilipi 4:19 tunasoma hivi; “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu”.

            Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua madhaifu yetu na magonjwa yetu yote, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona (Isaya 53:5; Mathayo 8:16, 17; 1Petro 2:24). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na kuombea wagonjwa na kutoa huduma za afya kwa wagonjwa.

            Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua dhambi zetu na akafanyika dhambi kwa ajili yetu, “Ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye” (2 Wakorintho 5:21). Na kwa kujua hili kanisa linahubiri habari za ondoleo la dhambi kwa ye yote atakayemwamini Kristo.

            Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alikuwa maskini, ingawa alikuwa tajiri, ili kwa umaskini wake sisi tupate kuwa matajiri (2Wakorintho 5:21). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili mtu aondokane na umaskini. Wakristo binafsi pia wanashauriwa kuwa na miradi isiyovunja maadili ya kikristo, ili waondokane na umaskini.

0 comments:

Post a Comment

Popular Posts

Recent Posts

Unordered List

Text Widget

Powered by Blogger.
Copyright © RAPHAEL KILALE | Powered by Blogger
Design by Saeed Salam | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com